Kwa mujibu wa Idara ya tarjama ya Shirika la Habari la Hawza, Bodi ya Wakurugenzi ya Mkusanyiko wa Wanazuoni wa Kiislamu wa Lebanon, katika bayana yake baada ya kikao chake cha kawaida imetangaza kuwa; siku hizi zinalingana na kumbukumbu ya mwaka wa kuuawa kishahidi makamanda mashahidi, Sayyid Abbas Mousawi, Sheikh Ragheb Harb na Hajj Imad Mughniyeh; watu waliotoa mchango mkubwa katika safari ndefu ya jihadi na muqawama. Makamanda hawa wanajivunia kuwa waanzilishi wa muqawama ulioanza kutoka sifuri na bila nyenzo zozote za maana; wakati ambapo adui Mzayuni aliikalia Lebanon na kufika hadi mji mkuu Beirut, mistari ya ulinzi iliporomoka na muqawama wa Palestina ukatoka Lebanon na, chini ya miradi ya maridhiano, ukaangukia katika mpango wa kujisalimisha uliomalizika kwa makubaliano ya fedheha kama Makubaliano ya Oslo. Hata hivyo, makamanda hawa walikuwa na mtazamo mwingine; walitegemea silaha ya imani na azma ya ushindi, na kwa kufanikisha ushindi mfululizo wakapata ushindi wa wazi dhidi ya adui Mzayuni na kumlazimisha kujiondoa tarehe 25 Mei 2000 (5 Khordad 1379 H.S).
Katika muendelezo wa bayana hiyo imeelezwa kuwa: Baada ya adui Mzayuni kujaribu kulipiza kisasi cha kushindwa kwake kwa fedheha katika vita vya mwaka 2006 (1384 Hijria Shamsia), Hajj Imad Mughniyeh chini ya uongozi wa Sayyid wa Mashahidi wa Umma, Sayyid Hassan Nasrallah, aliwashinda na ushindi mwingine ukapatikana. Ushindi huu uliweka mlingano mpya wa “mizania ya hofu” dhidi ya adui; mizania ambayo kwa muda wa miaka 18 ilimlazimisha kubaki katika hali ya kujizuia.
Mkusanyiko wa Wanazuoni wa Kiislamu umeongeza: Leo, baada ya makabiliano makubwa katika operesheni ya “Tufani al-Aqsa”, imebainika kuwa; adui Mzayuni hana kinga na anaweza kushindwa; kwani mamia ya wapiganaji wa muqawama wa Palestina waliweza kupenya katika makazi ya walowezi wa adui, kuwateka mateka na kuikomboa ardhi – hata kama kwa saa chache. Kufuatia tukio hilo, dunia yote ikiongozwa na Marekani ilikimbilia kuunga mkono utawala wa Kizayuni; wakati muqawama wa Kiislamu wa Lebanon, uliowekewa misingi na makamanda hao mashahidi, uliisimama kuinga mkono kambi ya Ghaza na ukaingia katika vita virefu. Katika vita hivyo, utawala wa Kizayuni kwa msaada wa moja kwa moja wa Marekani, uliwauwa makamanda wakuu wa muqawama, miongoni mwao ni shahidi mtukufu Sayyid Hassan Nasrullah na shahidi Sayyid Hashem Safi al-Din. Adui alidhani kuwa muqawama umevunjika, lakini ustahimilivu wa vijana wa Imad Mughniyeh katika vijiji vya mpakani mwa Palestina katika vita vya “Uli al-Ba’s” ulithibitisha kuwa muqawama bado una nguvu, heshima na mamlaka. Licha ya pigo zito na chungu, wana uwezo wa kurejesha mpango wa hatua, na kwa sasa wanatekeleza mkakati wa subira kama utangulizi wa vita vya maamuzi; vita ambavyo mwisho wake utakuwa ni kuangamia kikamilifu utawala wa Kizayuni.
Katika bayana hiyo imesisitizwa kuwa: Katika kumbukumbu ya makamanda mashahidi, tunatangaza kuwa, muqawama wa Kiislamu bado upo uwanjani kwa nguvu na unajiandaa kwa vita vya maamuzi; vita ambavyo havipo mbali, hasa kwa kuendelea kwa ukiukaji wa usitishaji mapigano na Azimio 1701 na adui Mzayuni.
Radi amali kutokana na uchokozi wa hivi karibuni
Mkusanyiko huu pia umelaani kitendo cha adui Mzayuni kumlenga kijana Muhammad Hussein Qashaqish; shambulio lililofanywa asubuhi ya leo na ndege zisizo na rubani za kivita katika njia ya kuwasafirisha wanafunzi kutoka mji wa Hanin, na kusababisha kuuawa kwake shahidi.
Katika sehemu nyingine ya bayana hiyo imeelezwa kuwa: Mkusanyiko huo pia umelaani shambulio la utawala wa Kizayuni dhidi ya gari katika barabara ya al-Masna’a lililosababisha kuuawa kwa watu wanne, na kusisitiza kuwa, ongezeko hili hatari linahitaji msimamo madhubuti na wa dhati wa serikali ya Lebanon ili kuzuia kurudiwa uhalifu kama huu.
Uchokozi ndani ya Palestina na Syria
Mkusanyiko wa Wanazuoni wa Kiislamu, huku ukilaani vitendo vya hivi karibuni vya utawala wa kikaliaji, umetangaza: Vikosi vya Israel kwa kutoa notisi za kubomoa nyumba kumi katika mji wa Tuqu’ katika mkoa wa Bethlehem, na pia kwa kufanya mashambulizi ya anga kaskazini na kusini mwa Ghaza, vimesababisha kuuawa kwa watu kumi na kujeruhiwa kwa raia kadhaa wa Kipalestina. Bayana hiyo imezitaka nchi wadhamini wa makubaliano ya Ghaza kuuzuia utawala wa Kizayuni kuendelea kukiuka makubaliano hayo.
Mwisho, Mkusanyiko wa Wanazuoni wa Kiislamu pia umeeleza kuwa; kitendo cha utawala wa Kizayuni kupenya katika kijiji cha “al-Mushayrifah” katika viunga vya Quneitra nchini Syria, sambamba na kuruka ndege za kijasusi zisizo na rubani juu ya eneo hilo, ni ukiukaji wa wazi wa mamlaka ya Syria, na kuwataka wahusika wenye mamlaka katika eneo hilo kusimamisha uchokozi huu kwa nguvu zote na kulinda usalama wa raia wa Syria. Bayana hiyo pia imeongeza kuwa: Ni wajibu kwa vikosi vya wananchi kuunda muqawama wa uwanjani ili kumzuia Mzayuni kurudia mashambulizi.
Maoni yako